Baba Yetu, Zaburi na sala nyingine za Biblia ili usali kwa maneno yake yenyewe.
Baba Yetu
9“Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. 10Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni. 11Utupatie riziki yetu ya kila siku. 12Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu. 13Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen.’
1Zaburi ya Daudi. Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. 2Hunilaza katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji matulivu huniongoza, 3hunihuisha nafsi yangu. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4Hata kama nikipita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami; fimbo yako na mkongojo wako vyanifariji. 5Waandaa meza mbele yangu machoni pa adui zangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, kikombe changu kinafurika. 6Hakika wema na upendo vitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
1Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba. Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu. 2Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu. 3Kwa maana ninajua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima. 4Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako, ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo, na kuwa na haki utoapo hukumu. 5Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. 6Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima. 7Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. 8Unipe kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda na ifurahi. 9Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote. 10Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu. 11Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu. 12Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze.
1Wimbo wa kwenda juu. Nayainua macho yangu nitazame vilima, msaada wangu utatoka wapi? 2Msaada wangu hutoka kwa Bwana, Muumba wa mbingu na dunia. 3Hatauacha mguu wako uteleze, yeye akulindaye hatasinzia, 4hakika, yeye alindaye Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi. 5Bwana anakulinda, Bwana ni uvuli wako mkono wako wa kuume, 6jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku. 7Bwana atakukinga na madhara yote, atayalinda maisha yako, 8Bwana atakulinda unapoingia na unapotoka, tangu sasa na hata milele.
1Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. 2Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali. 3Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote. 4Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana. 5Umenizunguka nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu. 6Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia. 7Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. 9Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari, 10hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti. 11Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,” 12hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
1Zaburi ya Daudi. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. 2Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usisahau wema wake wote, 3akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote, 4aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma, 5atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
1Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi. 2Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.” 3Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua. 4Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako. 5Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana, 6wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri.
1Zaburi ya Daudi. Wakati alipokuwa katika Jangwa la Yuda. Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji. 2Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako. 3Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha. 4Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
1Kisha Hana akaomba na kusema: “Moyo wangu wamshangilia Bwana, katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu. Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako. 2“Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Bwana, hakuna mwingine zaidi yako; hakuna Mwamba kama Mungu wetu. 3“Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, kwa kuwa Bwana ndiye Mungu ajuaye, na kwa yeye matendo hupimwa. 4“Pinde za mashujaa zimevunjika, lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu. 5Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe ili kupata chakula, lakini wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Mwanamke yule aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi amedhoofika. 6“Bwana huua na huleta uhai, hushusha chini mpaka kaburini na hufufua. 7Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha, hushusha na hukweza. 8Humwinua maskini kutoka mavumbini na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; huwaketisha pamoja na wakuu na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima. “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana; juu yake ameuweka ulimwengu. 9Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake, lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza. “Si kwa nguvu mtu hushinda; 10wale wampingao Bwana wataharibiwa kabisa. Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni; Bwana ataihukumu miisho ya dunia. “Atampa nguvu mfalme wake, na kuitukuza pembe ya mpakwa mafuta wake.”
46Naye Maria akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, 47nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu, 48kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa, 49kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu. 50Rehema zake huwaendea wale wamchao, kutoka kizazi hadi kizazi. 51Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao. 52Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi, lakini amewainua wanyenyekevu. 53Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu. 54Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu 55Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.”
6Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo. 7“Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
10Daudi akamhimidi Bwana mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele. 11Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee Bwana, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. 12Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe utawalaye vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, 13Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu.
17Ingawa mtini hauchanui maua na hakuna zabibu juu ya mizabibu, ingawaje mzeituni hauzai, na hata mashamba hayatoi chakula, iwapo hakuna kondoo katika banda, wala ngʼombe katika zizi, 18hata hivyo nitashangilia katika Bwana, nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu. 19Bwana Mwenyezi ni nguvu yangu; huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala, huniwezesha kupita juu ya vilima. Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.
39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”
20“Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
14Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu. 20Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.
9Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, 10ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, 11mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.
9Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru.
24Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.